Rais William Ruto ameagiza Shirika la Huduma ya Wanyamapori nchini (KWS) kutenga asilimia 40 ya nafasi wakati wa kuajiri walinzi kwa jamii zinazohifadhi mbuga za kitaifa katika mpango wake mpya wa utendakazi.
Akihudhuria ibada katika uwanja wa Mwatunge huko Taita Taveta mnamo Jumapili, Julai 23, Ruto aliagiza wakaazi 600 kutoka kaunti hiyo kupewa kipaumbele wakati wa kuajiri kujaza nafasi 1,500 zilizokuwa wazi.
Alibainisha kuwa utaratibu huo huo utatumika katika kaunti zingine ambazo ni wenyeji wa Hifadhi za Kitaifa.
Zaidi ya hayo, Mkuu wa Nchi aliagiza KWS kubuni mkakati ambao utaifanya Taita Taveta kuhifadhi nusu ya mapato yanayotokana na mbuga za wanyama.
“Kwa sasa, nakubaliana na viongozi wenu kwamba Taita Taveta hainufaiki na Hifadhi za Kitaifa. Kufikia mwaka huu, pesa zote zinazopatikana kutoka kwa mbuga za kitaifa zitagawanywa kwa nusu kumaanisha kuwa nusu itarejea kaunti huku nusu nyingine ikienda kwa serikali ya kitaifa,” akasema.
+ There are no comments
Add yours