HOSPITALI ya Mafunzo na Rufaa ya Moi (MTRH) imemulikwa kwa kuajiri zaidi ya asilimia 70 ya wafanyakazi kutoka jamii moja.
Hii ilifichuka mnamo Jumamosi baada ya Afisa Mkuu Mtendaji Dkt Philip Kirwa kuhojiwa na Kamati ya Bunge la Kitaifa kuhusu Uwiano na Fursa Sawa.
Dkt Kirwa alijikuna kichwa alipotakiwa kueleza kwa nini wafanyakazi wengi walikuwa wa jamii ya Wakalenjin.
Kikao hicho kiliongozwa na Mwenyekiti wa kamati Paul Nzengu, Mbunge wa Mwingi Kaskazini.
Wabunge hao waligundua taasisi hiyo ilikiuka Sehemu ya 7(1) na (2) ya Sheria ya Uwiano na Ushirikishi wa Kitaifa ya 2008.
Kulingana na sheria za ajira, taasisi za umma hazifai kuwa na wafanyakazi zaidi ya thuluthi moja kutoka kwa kabila moja.
Sajili ya mishahara na wafanyakazi ilionyesha kuwa hospitali hiyo ina wafanyakazi 3,632 na kati yao 2,551 ni Wakalenjin.
+ There are no comments
Add yours