Liverpool imedumisha ushindi wa mechi tatu mfululizo kwenye Ligi ya EPL baada ya kuitinga Manchester United 3 – 0 uwanjani Old Trafford Jumapili.
Luis Diaz alifunga mabao mawili katika kipindi cha kwanza na Mohamed Salah kipindi cha pili kuleta ushindi huo ugenini.
Diaz alitanguliza Liverpool dakika ya 35 kwa kichwa chake baada ya pasi ya Salah kutokana na Casemiro kufanya kosa na kutuma pasi mbovu ambayo Ryan Gravenberch alipata na kumpa Salah.
Casemiro alifanya kosa tena ambapo Diaz alimpokonya mpira na kupiga pasi kwa Salah kabla ya kukimbia mbele ya goli na Salah akampa tena pasi na mchezaji huyo wa Colombia akafunga bao la pili dakika ya 42.
Salah alifunga bao la tatu dakika ya 56 baada ya pasi ya Dominik Szoboszlai kabla ya kusukuma tobwe la chini.
Ushindi huo ulipandisha Liverpool hadi nambari ya pili na alama tisa sawa na Manchester City walio ya kwanza kwa kufunga mabao mawili zaidi. United wako nambari ya 14 na alama tatu.
+ There are no comments
Add yours