Mshukiwa wa dawa za kulevya Yusuf Ahmed Swaleh almaarufu Candy Rain alipatikana Jumapili akiwa amefariki katika eneo la Vipingo, Kaunti ya Kilifi.
Polisi walisema alipatikana amefariki Jumapili, Machi 17 mjini Kilifi siku chache baada ya kutekwa nyara na watu wasiojulikana. Anasemekana kurithi himaya ya mihadarati ya Akasha huko Pwani.
Kulingana na tarifa ya wakili wake, watu waliojitambulisha kuwa maafisa wa polisi walifika mlangoni kwake na kumwambia Swaleh kuwa walihitaji kumhoji na kumchukua siku tisa zilizopita. Inaaminika kuwa Swaleh aliuawa muda mfupi baada ya kutekwa nyara.
Inasemekana kuwa Swaleh amekuwa kinara wa ulanguzi wa dawa za kulevya Pwani kufuatia kufikishwa kwa ndugu wa Akasha nchini Marekani kwa tuhuma za ulanguzi wa dawa za kulevya.
Kifo cha mshukiwa wa dawa za kulevya kinajiri takriban mwezi mmoja baada ya serikali ya kitaifa kutangaza vita dhidii ya dawa za kulevya Pwani.
Akiwa katika ziara ya kikazi mkoani humo, Inspekta Jenerali wa Polisi, Japhet Koome alitoa agizo kwa polisi kumkamata mfanyabiashara wa dawa za kulevya. Pia aliwafanyia mabadiliko mabosi wa polisi wa mikoa ya Mkoa wa Pwani kwa kueleza kuwa bosi wa awali alishindwa kudhibiti biashara ya mihadarati.
+ There are no comments
Add yours